Bunge Maalum la Katiba giza nene

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta,
Bunge Maalumu la Katiba, ambalo vikao vyake vinatarajiwa kuendelea kesho limegubikwa na giza nene kufuatia mvutano mkubwa unaoendelea baina ya wajumbe wake na hivyo kutishia mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya.
Hali hiyo inatokana na wajumbe hao kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuendelea kurushiana vijembe nje ya Bunge hilo.
Aidha, wajumbe wa Ukawa wameendelea na msimamo wao wa kususia kushiriki vikao vya Bunge hilo na hivyo, kuzidi kuongeza hofu juu ya ugumu wa upitishaji wa vifungu vya rasimu ya katiba katika Bunge hilo.
Kutokana na hali hiyo, wajumbe hao jana walitakiwa kujadili katika Bunge hilo rasimu ya katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kama wana nia ya kuipatia nchi katiba mpya.
Ushauri huo ulitolewa jana na wataalamu wa Kitengo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika kongamano lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo hicho (Udasa).
Akizungumza katika kongamano hilo, Profesa Gaudens Mpangala, alisema utafiti uliofanywa na Tume iliyoundwa na Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) kufuatilia Mchakato wa Katiba nchini, uligundua mchakato huo ulikwama kutokana na kuhusishwa na maslahi ya kisiasa.
Alisema tume hiyo ilibaini mambo, ikiwamo kutozingatiwa kwa maoni yaliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kuponda rasimu ya katiba, lugha za matusi kutoka kwa baadhi ya wajumbe pamoja na uzinduzi wa Bunge.
Mwakilishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, alisema hoja siyo serikali tatu tu, bali ni pamoja na wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulifanya Bunge hilo kuwa mkutano wa CCM.
Kwa upande wake, mwakilishi wa CCM, Steven Wassira, alisema kilichowashinda kujenga hoja zitakazokishawishi chama tawala ni kukubali mfumo wa serikali tatu.
Katibu Mwenezi wa Taifa TLP, Dominata Rwechungura alisema haoni haja ya kuendelea na mchakato wa Bunge Maalum la Katiba, endapo Ukawa hawatarejea Bungeni na kusema ni vyema Bunge hilo lihairishwe.
Alisema upatikane muafaka kwanza ndipo Bunge hilo liendelee kuliko kuendelea kwa mjadala na fedha nyingi kutumika katika shughuli hiyo pekee.
“Ni bora fedha hizo zikaelekezwa katika shughuli za maendeleo katika afya, elimu na maeneo mengine. Hakuna haja ya Bunge kuendeshwa bila kuwa na uwiano,” alisema Rwechungura.
CHIMBUKO LA MGOGORO
Aprili 16, mwaka huu, wajumbe wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliusia kikao cha Bunge hilo kwa madai ya upendeleo na ubaguzi uliokuwa unafanywa na Chama Cha Mapinduzi dhidi ya vyama vingine.
Wajumbe hao wanaounda umoja huo kutoka vyama vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na wa vyama vingine, walichukua hatua hiyo pia wakituhumu kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, waliyodai kuwa ni za ubaguzi na vitisho akiwa kanisani kwamba Wazanzibari wanaotaka serikali tatu wanataka ijitenge ili iwe nchi ya Kiislamu.
Msimamo huo ulitolewa siku hiyo jioni na Profesa Ibrahim Lipumba alisema kuwa Lukuvi alitoa kauli hiyo mkoani Dodoma katika Kanisa la Methodist wakati wa sherehe za kumsimika Askofu Joseph Bundara wa Jimbo la Dodoma
Profesa Lipumba alisema kwamba Lukuvi aliyemwakiisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alizungumza lugha ya vitisho ndani ya kanisa kwamba kama serikali tatu zitaundwa na serikali ya Muungano ikashindwa kuwalipa mshahara wanajeshi, Jeshi litachukua nchi
Alisema kuwa kauli hizo zilisababisha Askofu Bundara kusema kwamba ni vema Katiba ya Zanzibar ikafutwa na kuundwa katiba moja.
Lipumba alisema Bunge limegeuka kuwa Interahamwe akimaanisha wanamgambo waliochochea ubaguzi na kusababisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni muumini ya dini ya mwenyezi Mungu, lakini naafiki mapendekezo yaliyoletwa kwetu na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ni Tume iliyoundwa na Rais.
“Na waziri Lukuvi alikuwa anamwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda…Mheshimiwa hii inasikitisha na inasikitisha kwa kuwa kauli hii pia inafanana na kauli ambayo Rais Jakaya Kikwete aliitoa wakati akitoa hotuba katika bunge hili,” alisema.
“Hii ni Rasimu ya Tume ya Rais na si rasimu ya Wapemba, lakini katika mjadala wetu hapa umekuwa na utaratibu wa ubaguzi, watu wamebaguliwa humu na viongozi wakubwa wanapiga makofi, Bunge hili limekuwa kama Bunge la ‘Intarahamwe’, hii ni hatari kwa nchi yetu,
“Wapemba, Waarabu, Wahindi, Wakongo, hii hatuitaji katika nchi yetu, tunahitaji katiba ambayo itahakikisha kila mwananchi anapata haki yake wote tuwe sawa, bila kujali, rangi zetu, makabila yetu, dini zetu, hii ndiyo nchi aliyotuachia Mwalimu Nyerere,” alisema.
“Kutokana na hali hii, tumechoka kusikiliza matusi, tumechoka kudharau mawazo ya wananchi, tumechoka ubaguzi, hatuwezi kuwa sehemu ya kundi la Interahamwe linalohamasisha ubaguzi ndani ya Tanzania…hili hatulikubali, hatulikubali, tunawaachia, watu wote tunaotaka katiba ya wananchi tunawaachia Interahamwe muendelee na kikao chenu,” alisema.
“Hatuwezi kuwa sehemu ya Interahamwe,” alisema Profesa Lipumba na baada ya kumaliza kuzungumza, wajumbe wote wa Ukawa na wengine walisimama na kuondoka ndani ya ukumbi huku wakipiga kelele.
Baada ya kutoka nje ya ukumbi wa Bunge huku wajumbe wa kundi hilo linalojumuisha vyama vya hivyo pamoja na NLD kinachoongozwa na Dk. Emmanuel Makaidi, DP kinachoongozwa na Mchungaji Christopher Mtikila na baadhi ya wajumbe wa kundi la 201, huku wakiimba nyimbo mbalimbali. “Tunaondoka, tunawaacha Interahamwe, Interahamwe.”
LUKUVI NA KANISA
Alitaja sababu nyingine iliyowafanya watoke nje ya ukumbi wa Bunge wakati mjadala ukiendelea ni hatua ya Lukuvi kuzungumza ndani ya kanisa, akieleza kuwa ulikuwa ni makakti maalum wa kuwabana Wazanzibari.
Profesa Lipumba alisema wanaweza kurudi endapo tu mambo yatakayokuwa yakijadiliwa ni yale tu yaliyomo katika Rasimu iliyopendekezwa na Tume ukiwamo muundo wa Muungano wa serikali tatu.
KIKWETE
Akihutubia Taifa Agosti Mosi, mwaka huu, katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi, Rais Kikwete alisema hivi karibuni amekuwa akilaumiwa kuwa mambo yalikuwa yanaenda vizuri mpaka pale alipotoa hotuba ya ufunguzi wa Bunge Maalumu ndipo yalipoharibika.
Pia alisema amekuwa akilaumiwa kwamba anawezaje kuikana rasimu ya katiba, ambayo na yeye alikuwa ni mmoja wa watu waliotia sahihi katika rasimu hiyo.
Akijibu madai hayo, Rais Kikwete alisema wanaotoa madai hayo wameitafsiri isivyo sahihi yake katika Gazeti la Serikali lililotangaza rasmi rasimu ya katiba na Taarifa ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba baada ya Tume kumaliza kazi yake ya kuandika Rasimu ya Katiba, Rais wa Jamhuri ya Muungano amepewa kazi tatu kufanya.
Alizitaja kazi hizo kuwa ni kupokea Rasimu hiyo na Taarifa ya Tume kutoka kwa Mwenyekiti, kuitangaza rasmi Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume kwa watu wote kuiona na kuisoma ndani ya siku 30 na kuitisha Bunge Maalumu.
MADHARA KWA THELUTHI MBILI
Ikiwa hawatarejea bungeni wataathiri upitishaji wa katiba kwa sababu kanuni namba 36 (1) bila kuathiri masharti ya sheria na kanuni hizi, mapendekezo ya marekebisho, au mabadiliko yaliokidhi matakwa ya na masharti ya kanuni hizi kuhusu sura za rasimu ya katiba zinazohusika yatajadiliwa na kupigiwa kura ibara kwa ibara katika kipindi kisichozidi siku moja.
Ibara ya 2 inasema mapendekezo ya marekebisho au mabadiliko yaliyowasilishwa kwa mujibu wa fasiri ya (1) yatapigiwa kura na kupitishwa kwa kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar.
Ibara ya 3 inasema pale mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko yatakubaliwa, ibara inayohusika ya rasimu ya katiba itahesabiwa kuwa imepitishwa pamoja na mabadiliko yake isipokuwa kwamba pale ambako mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko yatakataliwa, ibara inayohusika ya rasimu ya katiba itapigiwa kama ilivyokuwa kwa kufuata masharti ya fasiri ya (2).
Ibara ya Nne, endapo baada ya kupigiwa kura, theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar haikufikiwa, basi ibara hiyo itapelekwa kwenye kamati ya mashauriano ili kupata muafaka.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, inawatambua wajumbe wote waliokula kiapo na ndiyo sababu baadhi ya kamati miongoni mwa 12, zilizochambua rasimu zilishindwa kupitisha maamuzi kutokana na kukosa theluthi kwa pande zote wakati wa kupiga kura kutokana na baadhi ya wajumbe kutokuwapo.
CHANZO:
NIPASHE
Maoni
Chapisha Maoni